IQNA

Wanafunzi Marekani waandamana kujibu barua ya ubaguzi iliyolenga Waislamu

15:45 - March 29, 2024
Habari ID: 3478600
IQNA - Wanafunzi wengi katika Chuo Kikuu cha Washington (UW) huko Seattle nchini Marekani wameandamana kupinga ubaguzi na chuki dhidi ya Waislamu.

Maandamano ya Alhamisi yalifuatia barua ya chuki iliyotumwa hivi majuzi kwa Jumuiya ya Wanafunzi Wasomali wa Chuo Kikuu cha Washington ambao ni Waislamu. Lugha hiyo ya kibaguzi ilizua mwito wa kuchukua hatua kuwalinda wanafunzi.

"Inasikitisha  kuona chuki dhidi ya Waislamu, haswa katika wakati  Waislamu wengine wanaedelea kuteseka katika nchi zingine kama Palestina," mwanafunzi mmoja, ambaye alificha utambulisho wake kwa usalama wake.

Wakati wa maandamano hayo, baadhi ya wanafunzi walisema wanakumbwa na chuki chuoni kwa sababu ya dini yao na kwamba chuo kikuu kilikuwa kimechelewa kuwaunga mkono.

"Ukweli kwamba tunapaswa kufanya maandamano kama haya, ili kuleta ufahamu, ni ishara ya kiasi gani chuo kikuu kinafanya. Nadhani tunapaswa kuwasukuma zaidi kidogo ili kuhakikisha wanajua kuwa hatujisikii kuungwa mkono," mwanafunzi wa pili alisema.

Wanafunzi hao walisema walikuwa na wasiwasi kuhusu kulengwa ikiwa watafichua utambulisho wao. Hofu yao inakuja siku chache baada ya barua za chuki kutumwa kwa Jumuiya ya Wanafunzi wa Kisomali chuoni hapo, ikiwaambia wanafunzi "kurudi walikotoka," na "hatuhitaji Waislamu, waasi, magaidi, au wakomunisti hapa UW."

Maafisa wa UW walisema polisi wa chuo kikuu na watekelezaji sheria wa eneo hilo walikuwa wakichunguza barua hiyo, wakisema hakuna mahali pa unyanyasaji au ubaguzi katika chuo kikuu. Wakati wa maandamano hayo, wanafunzi walisema wanataka viongozi wa UW kuthibitisha hilo na kusimama pamoja nao.

Katika taarifa iliyoandikwa, maofisa wa UW walisema, "tutafuata kila njia iwezekanayo kutambua na kumwajibisha mtu yeyote aliyetekeleza vitendo dhidi ya wanafunzi wetu, kitivo au wafanyikazi."

Tawi la Washington la Baraza la Mahusiano ya Kiislamu ya Marekani (CAIR-WA), ilitoa wito kwa Chuo Kikuu cha Washington kuzungumza dhidi ya kipande cha barua ya chuki iliyotumwa kwa wanafunzi hao Waislamu.

3487741

captcha