IQNA

Shakhsia katika Qur'ani Tukufu / 31

Nabii wa Mwenyezi Mungu ambaye pia alikuwa Mfalme, Mwanachuoni na Hakimu

19:42 - February 13, 2023
Habari ID: 3476555
TEHRAN (IQNA) – Dawod alikuwa miongoni mwa Mitume wakubwa wa Mwenyezi Mungu miongoni mwa Bani Isra’il ambaye pia alikuwa mfalme, hakimu na mwanachuoni msomi.

Dawod (AS), aliyeishi karibu karne ya 10 Kabla ya Nabi Isa (AS), alikuwa mwana wa Isha, wa ukoo wa Yuda, mwana wa Yakub (AS). Alizaliwa katika ardhi kati ya Misri na Sham na akawa mmoja wa manabii wakubwa wa Bani Isra’il.

Baada ya Talut, kamanda wa Bani Isra’il, kuahidi kwamba atatoa nusu ya mali yake na kumuozesha binti yake kwa yeyote anayeweza kumshinda Jalut, Dawod aliweza kumuua Jalut kwa jiwe kwenye kombeo lake na kumlenga. Dawod pia aliiteka al-Quds (Jerusalem) na kuifanya mji mkuu wa serikali ya Bani Isra’il.

Dawod (AS) alikuwa kwa wakati mmoja nabii na mfalme wa Bani Isra’il. Hali hii ilikuwa nadra sana kwa manabii wa Mwenyezi Mungu.

Qur'ani Tukufu inataja jina la Dawod mara 16, ikijumuisha katika Sura An-Naml, Al-Isra, Al-Anbiya, na Saad. Kwa mujibu wa aya hizi na pia Hadithi, kumekuwa na sifa tofauti zinazonasibishwa kwa Dawod. Kulingana na aya za Qur'ani Tukufu, Dawod (AS)  alijua lugha ya wanyama. Mwenyezi Mungu alimpa nguvu na ujuzi na kumfundisha yale aliyotaka kujifunza, kutia ndani jinsi ya kutengeneza silaha na jinsi ya kuhukumu kati ya watu.

Pia inasemekana alitumia wakati mwingi kumwabudu Mwenyezi Mungu na pia alikuwa na sauti nzuri na alimwomba Mola kwa sauti yake nzuri.

Jina la kitabu kitakatifu cha Dawod ni Zaburi. Kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu na Hadith, kitabu cha Zaburi kiliteremeshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Inajumuisha mfululizo wa ushauri na mapendekezo, ujuzi na maombi. Qur'ani Tukufu inataja jina la Zabur mara tatu katika Sura An-Nisa, Al-Anbiya, na Al-Isra. Zaburi ni kitabu cha saba cha Agano la Kale ambacho kinajumuisha dua150.

Nabii Dawod ana hadhi maalum miongoni mwa Wayahudi ingawa baadhi ya tuhuma zimetolewa dhidi yake ambazo hazina msingi kwa mujibu wa Uislamu.

Dawod alikuwa na watoto 19 na mtoto wake, Suleiman, alimrithi kwa amri ya Mungu.

Nabii Dawod alifariki akiwa na umri wa miaka 100 na baada ya miaka 40 ya kuwatawala Bani Isra’il. Baada ya kifo chake, wanazuoni 40,000 wa Bani Isra’il na watu mashuhuri walihudhuria mazishi yake na akazikwa huko Al Quds.

captcha