IQNA

Shakhsia katika Qur'ani Tukufu /33

Ushauri wa Kibaba wa Luqman kwa Mwanawe

17:32 - February 28, 2023
Habari ID: 3476637
TEHRAN (IQNA) – Luqman alikuwa mwanachuoni aliyeishi zama za Nabii Dawoud na alijulikana kwa elimu yake kubwa, hekima na ushauri wake wa kimaadili kwa mwanawe.

Kuna maoni tofauti juu ya hulka yake njema. Wengine wanasema alikuwa msomi mkubwa na mtu wa maadili. Wengine wanaamini alikuwa Nabii wa Mwenyezi Mungu. Kulingana na baadhi ya watu wengine, alikuwa mtumwa aliyefikia hadhi ya juu sana ya kiroho kutokana na sifa zake nzuri za kimaadili na kwa hiyo bwana wake alimwacha huru.

Pia kuna maoni tofauti kuhusu rangi yake na mahali alipoishi. Wengine wanaamini kuwa alitokana na watu wa Aad, na wengine wanasema alitoka Bani Isra’il. Kuna wengine wanasema alikuwa mtumwa kutoka Abyssinia (Ethiopia ya leo).

Luqman alikuwa mhusika ambaye alimsaidia Mtume Dawoud (AS) katika masuala ya mahakama.

Miongoni mwa sifa zake zilikuwa unyenyekevu mbele ya watu, kutosonga kamwe kuelekea ushirikina, kutembea polepole, muelekeo wa wastani katika maisha, kufikiri kwa kina, ukimya, uaminifu, ukweli na kusaidia kutatua mizozo ya watu.

Kuna Sura katika Qur'ani Tukufu inayoitwa Luqman ambayo inataja vipande kumi vya nasaha zake kwa mwanawe. Nasaha hizo zinasisitiza haja ya subira nyakati za magumu, kusali, kuhimiza mema na kuzuia maovu, na kuwa na muelekeo wa wastani maishani.

Nasaha zake pia zimetajwa katika vitabu vya dini. Kwa mfano, alimsihi mwana wake awasaidie watu, sikuzote atabasamu, awe mkarimu, akubali mialiko ya wengine, na kushauriana na marafiki zake.

Luqman aliamini kuwa sahaba mwema ni mtu anayemkumbuka Mungu daima. Matendo ya mtu wa namna hiyo huwanufaisha wenezake na kuleta rehema ya Mwenyezi Mungu.

Pia aliamini hata marafiki elfu moja hawatoshi huku adui hata moja akiwa ni sawa na maadui wengi sana.

Luqman alikuwa binadamu wa kawaida ambaye alikuwa na ufahamu mkubwa na uwezo wa kiakili. Imepokewa kwamba mmoja wa marafiki zake alimuuliza ni kwa namna gani alipata elimu nyingi hivyo na akajibu kuwa ni baraka za Mwenyezi Mungu na akapewa sifa zake kama vile uaminifu, ukweli na ukimya wakati hakuna faida katika kuzungumza.

captcha