IQNA

Matembezi ya Arbaeen

Nasrallah asema Ushiriki wa wafanyaziara Milioni 20 katika Arbaeen ni Muujiza

18:40 - September 17, 2022
Habari ID: 3475799
TEHRAN (IQNA) – Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa ushiriki wa wafanyaziara wa Kiislamu wapatao milioni 20 katika matembezi ya Arbaeen nchini Iraq mwaka huu ni muujiza.

Sayyed Hassan Nasrallah aliyasema hayo katika hotuba yake ya televisheni iliyotangazwa moja kwa moja kutoka mji wa Baalbek mashariki mwa Lebanon siku ya Jumamosi kwa mnasaba wa Siku ya Arbaeen.

Nasrallah alielezea maandamano au matembezi ya Arbaeen nchini Iraq kama "maadhimisho ya kipekee" kulingana na ukubwa na idadi ya watu, na akasema tukio hilo ambalo limewashirikisha wafanyaziara  milioni 20 ni "muujiza."

"Arbaeen huko Karbala mwaka huu inachukuliwa kuwa mkusanyiko mkubwa zaidi ulimwenguni kwani idadi ya wafanyaziara walio katika mji huo mtakatifu inafikia milioni 20," mkuu wa Hizbullah alisema.

“Katika historia, hakuna mkusanyiko kama wa kukusanyika wapenzi wa Imam Hussein AS katika mji mtakatifu wa Karbala, na hii leo ni kama muujiza. Wafanyaziara milioni ishirini inamaanisha mioyo milioni 20 inapiga kwa ajili ya mapenzi ya Imam Hussein (AS).”

Nasrallah pia alitoa shukrani zake kwa vyama na mirengo yote ya kisiasa ya Iraq, na aliwashukuru watu wa Iraq kwa ukarimu wao.

Wafanyaziara  ambao aghalabu walivalia mavazi meusi kama ishara ya maombolezo walikusanyika katika haram tukufu ya Imam Hussein AS huko Karbala siku ya Jumamosi katika kilele cha matembezi ya zaidi ya wikki moja ya ukumbusho wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Mohammad (SAW), ambaye aliuawa shahidi pamoja na masahaba zake wakati wa vita vya Karbala mwaka 61 Hijria Qamaria au 680 Miladia.

Wanaume, wanawake, vijana na wazee walikusanyika kwa mamilioni katika mji huo wa Iraq ili kutoa heshima kwa Imam Hussein (AS), ambaye ni kiongozi na mbeba bendera ya vita dhidi ya dhulma na ukandamizaji.

Tukio hilo la kila mwaka, ambalo ni moja ya makusanyiko makubwa ya kidini duniani, huleta pamoja umati wa wapenzi na waumini wa Imam Hussein AS kutoka mataifa mbalimbali wanaofanya matembezi ya kilomita 80 kati ya miji mitakatifu ya Najaf na Karbala.

Ikumbukwe kuwa, siku kama ya leo miaka 1383 iliyopita, ilifanyika majlisi ya kwanza ya siku ya Arbaeen au Arubaini tangu kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW Imam Hussein bin Ali akiwa na wafuasi wake wakiwemo watu wa Nyumba ya Mtume SAW au Ahul Bayt. Waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria. Majlisi ya siku ya Arbaeen hufanyika kila mwaka baada ya kupita siku Arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume na masahaba zake watiifu ambao walijisabilia roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika ardhi ya Karbala.

4086051

Habari zinazohusiana
captcha