IQNA

Arbaeen 1435

Ujumbe wa Arbaeen ni mapambano kwenye njia ya haki

18:54 - August 30, 2023
Habari ID: 3477523
TEHRAN (IQNA) – Ujumbe wa Arbaeen ni kwamba lazima tujitahidi katika njia ya haki na kuhuisha ukweli katika hali zote.

Arbaeen ilikuwa na hadhi maalum miongoni mwa Maimamu wetu Watoharifu na Maasumin (AS), yaani Ahul Bayt wa Mtume Muhammad (SAW). Imamu Sadiq (AS) ana dua iitwayo Ziyarat al-Arbaeen na kwayo anawahimiza waumini kwenda katika safari au Ziara ya Arbaeen alikozikwa Imam Hussein (AS) katika mji wa Karbala nchini Iraq.

Ziara ya  kwanza ya Arbaeen ilitekelezwa wakati Jabir ibn Abdullah Ansari, ambaye alikuwa miongoni mwa masahaba wa Mtukufu Mtume (SAW) na alikuwa mzee sana wakati huo na alikuwa amepofuka, alikwenda Karbala na mmoja wa marafiki zake.

Tunapaswa kupokea jumbe za Arbaeen kutoka kwa Ziyarat al-Arbaeen wa Imam Sadiq (AS).

Imamu Sadiq (AS) alishauri kwamba siku ya Arbaeen waumini wasome sehemu hii ya dua: Assalamu Ala Walliyillah na Habibihi, Assalamu Ala Khalilillah na Najibihi, Assalamu Ala Safiallah na Ibn Saffiyih.

Sehemu ya kwanza ni salamu kwa Walii na rafiki wa Mwenyezi Mungu. Hadhi ya Imam Husein (AS) imewekwa wazi kwa ajili yetu katika dua hizi.

Walii ni yule ambaye amepewa Mamlaka na Mwenyezi Mungu na yeye pia ni Habib (rafiki) wa Mwenyezi Mungu na kwa hakika Mwenyezi Mungu anampenda. Najib maana yake ni mtukufu na mteule. Khalil ni hadhi ya Nabii Ibrahim (AS). Maimamu wetu (AS) hawazidishi chumvi. Wanaposema Imam Hussein (AS) ni Khalil wa Mwenyezi Mungu ina maana Imam Hussein (AS) amefikia hadhi hiyo.

Kisha tunasoma katika dua: Mungu! Nashuhudia kwamba yeye ndiye Walii Wako na mwana wa Walii Wako. Yeye ni mteule na Wewe ndiye uliyemchagu. Yeye ndiye uliyemheshimu na kusababisha kumfikia heshima uliyotaka afikie. Ulimfanya mkuu na ukampa heshima kwa kifo chake cha kishahidi.

Yazid na wafuasi wake walidhani kwamba kwa kumuua Imam Hussein (AS) wameweza kuwasahaulisha watu lakini Mwenyezi Mungu alimpa Imam Hussein (AS) heshima kwamba jina lake liko hai na litaendelea kuwa juu miongoni mwa Waislamu na wasiokuwa Waislamu hadi Siku ya Kiyama.

Yazid na watu wake walidanganywa na ulimwengu. Waliuza ukweli na haki kwa pesa kidogo na kubadilisha maisha yao ya akhera kwa pesa kidogo. Walimuua Imam Hussein (AS) ili kupata vyeo vya kidunia.

Ni ujumbe wa Arbaeen kwamba lazima tujitahidi kwa ajili ya kuhuisha na kushikilia ukweli katika hali zote. Harakati ya Ashura ipo siku zote. Harakati ya ukweli na harakati uongo zipo siku zote.

Ni muhimu tuepuke upotofu na tutofautishe ukweli na uwongo. Ilikuwa ni msiba ambao wakati huo watu hawakutofautisha ukweli na uwongo na wale waliofanya hivyo, walishindwa kusimama kwa ajili ya ukweli kutokana na tamaa zao za kidunia.

Inafaa kuashirikia hapa kuwa, Arbaeen ni neno la Kiarabu ambalo maana yake ni 40.  Katika muktadha huu, ni siku ya 40 tangu maadhimisho ya kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein (AS) na masahaba wake watiifu tarehe 10 Muharram katika siku ya Ashura. Mtukufu huyo aliuawa shahidi katika mapambano ya Karbala  karne 14 zilizopita.

Siku ya Imam Hussein (AS) ya Arbaeen inakuja tarehe 20 Safar, mwezi wa pili wa kalenda ya mwandamo wa Kiislamu.

Baada ya kufa shahidi Imam Hussein (AS) mikononi mwa katili Yazid bin Muawiya, watu ambao walishangazwa na ukatili wa ukoo wa Ummaya walianza kuzuru kaburi lake kutoa heshima zao na tokea wakati huo hadi leo vizazi katika umma wa Kiislamu vimeendeleza utaratibu huo. Kila mwaka idadi ya wafanyaziara katika Siku ya Arabeen inaongezeka ambapo mwaka uliopita idadi hiyo ilivunja rekodi na kufika milioni 21.

3484978

Habari zinazohusiana
captcha